Madhara 8 ya Kusikiliza au Kutazama Mziki

Madhara 8 ya Kusikiliza au Kutazama Mziki

Mziki
Kwa hakika kila jambo lenye uzuri au faida lina hasara zake. Nafahamu umekuwa ukisikia faida kede kede za kusikiliza mziki, lakini haujasikia kuwa kwa upande mwingine mziki unaweza kuwa na madhara kwako.
Ikiwa wewe ni mpenzi wa muziki, ni vyema ukafahamu madhara ya kusikiliza au kutazama mziki ili uutawale mziki usikuathiri.

1. Huathiri afya ya masikio

Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kumeibuka vifaa mbalimbali katika swala la utengenezaji, usambazaji na hata usikilizaji wa mziki.
Kutokea kwa teknolojia ya vifaa vya kusikilizia mziki vijulikanavyo kama headphones au earphones kumesababisha watu wengi hasa vijana kusikiliza mziki karibu kila mahali na kila wakati.
Taarifa mbalimbali za kitabibu zinaeleza kuwa vifaa hivi vimechangia sana kuharibu masikio au mfumo wa kusikia wa watumiaji wengi wa vifaa hivi; kwani wengi huvivaa siku nzima au usiku kucha.
Hivyo kusikiliza mziki sana hasa kwa kutumia headphones au earphones kunaweza kuathiri afya ya masikio yako, hivyo ni vyema kuwa na kiasi.

2. Huchangia kuharibu maadili

Miziki ya leo hasa ile inayofahamika kama miziki ya kizazi kipya, hujumuisha maudhui mengi ambayo ni kinyume cha maadili.
Katika miziki hii wasanii hutumia lugha chafu, huvaa mavazi ya aibu, au hata kufanya matendo ya aibu katika miziki iliyowekwa kwenye video.
Hili limesababisha watoto na vijana wengi kuiga tabia hizi ambazo kimsingi ni kinyume cha maadili mema. Hivyo kusikiliza au kutazama miziki hii kunaweza kuathiri maadili yako kama hutokuwa na utawala mzuri wa kifikra na kimaamuzi.

3. Huvuruga utendaji kazi

Kuna watu wanaosikiliza mziki kwa kiwango cha kupitiliza; watu hawa husikiliza mziki kazini, nyumbani, au hata darasani.
Swala hili linaweza kuathiri ufanisi wako kwani mara nyingi mziki utachangia kukusababisha usijikite kwenye kile unachopaswa kufanya.
Hebu fikiri mtu yuko darasani anamsikiliza mwalimu huku akiwa amevaa headphones au earphones; je ataweza kuelewa kweli kinachofundishwa? Ni wazi kuwa hatoweza kuelewa.

4. Huweza kusababisha ajali

Pamoja na mziki kufanya safari au uendeshaji wa gari usichoshe, mziki unaweza kusababisha ajali ikiwa hautatumika vyema.
Dereva awapo barabarani anapaswa kuhakikisha anasikia vyema mambo yanayoendelea barabarani, pia anapaswa kuweka akili yake kwenye uendeshaji wa gari lake.
Hivyo dereva anapaswa kuhakikisha hatekwi na mziki ulioko kwenye gari na kusahau chombo anachoendesha ili asije akasababisha ajali.

5. Huvunja mahusiano

Najua umeshajiuliza swali akilini mwako kuwa mziki unavunjaje mahusiano. Taarifa mbalimbali zinaonyesha kuwa watu wengi hupenda kufanya yale yanayoonekana au kuimbwa kwenye nyimbo mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa baadhi ya nyimbo huhamasisha watu kusalitiana—yaani kuwa na wapenzi wengi au kujihusisha kwenye maswala ya ngono kabla ya wakati.
Hivyo basi, mahusiano mengi yamevunjika kutokana na kuhadaiwa na maneno au tabia za wasanii; pia wengine wametengana pale ambapo mmoja wao hakuwa tayari kujihusisha kwenye maswala ya ngono.

6. Hupoteza muda

Ni ukweli kuwa mziki ni burudani nzuri na ya kipekee lakini inatakiwa kutumiwa kwa kiasi. Hebu fikiri mtu anasikiliza mziki siku nzima; hafanyi kazi, haongezi maarifa wala hapumziki.
Huku ni kupoteza muda ambao ungeweza kuutumia kwenye kufanya kazi nyingine zenye tija. Badala ya kukaa kwenye televisheni, redio au simu siku nzima ukisikiliza mziki, fanya kazi yenye tija au ongeza maarifa mapya.

7. Hupoteza pesa

Kuna baadhi ya watu hununua kila mziki mpya au hulipa pesa ili kusikiliza na kutazama miziki mbalimbali. Jambo hili ni upotevu wa pesa ambazo ungeweza kuzitumia kufanya mambo yenye manufaa zaidi kwako.
Badala ya kumaliza pesa zako kwenye miziki, anzisha angalau mradi mdogo ambao utawekeza pesa zako ili baadae zikuingizie faida.

8. Hukufanya kuwa mtumwa

Kuna watu wametekwa na mziki kiasi cha kutoweza kutengwa na mziki hata kwa dakika moja. Watu hawa utawakuta wakifuatilia na kusikiliza mziki kila mara au wakimfuatilia msanii fulani wa mziki.
Mara nyingi maisha au utendaji kazi wa watu hawa huingiliwa na huathiriwa na mziki kwa kiasi ambacho hawawezi kujinasua tena.
Si ajabu kwa watu hawa kuimba mziki barabarani, bafuni, au hata ndotoni au hata kugombana kwa ajili ya mziki au wasanii wanaowapenda.

Neno la mwisho
Kuwa na kiasi katika jambo lolote bila kujali ni zuri au laa ni jambo muhimu sana. Ingawa mziki unamanufaa mengi, ni vyema pia kufahamu madhara yake ili ujitahidi kuyaepuka.

Comments

Popular Posts