Loris Karius atumiwa salamu na Salah

Loris Karius atumiwa salamu na Salah


Mshambuliaji wa Liverpool Mohamed Salah amemwambia mchezaji mwenzake, mlinda lango Loris Karius "kuwapuuza wapenda chuki" baada yake kukosolewa zaidi kutokana na makosa aliyoyatenda wakati wa mechi ya kuanza kwa msimu.

Karius, 25, alidaiwa kusababisha bao la tatu la Borussia Dortmund katika mechi ambayo Liverpool walilazwa 3-1.

Kipa huyo alielekeza mkwaju kutoka kwa Christian Pulisic wa Dortmund kwenye njia ya Bruun Larsen aliyefunga bao lao la ushindi.

Kwa mujibu wa BBC, Karius alifanya kosa hilo siku chache baada yake kudaiwa kufanya kosa jingine mapema mwezi huu mechi ya kirafiki dhidi ya Tranmere.

Alishindwa kudhibiti vyema mpira wa frikiki aliokuwa ameudaka na kuwawezesha wenyeji kufunga wakati wa mechi hiyo iliyomalizika kwa ushindi wa Liverpool wa 3-2 uwanjani Prenton Park.

Liverpool walikuwa wameongoza 3-0 kufikia wakati wa mapumziko kupitia mabao ya Rafael Camacho, Sheyi Ojo na Adam Lallana, kabla ya Jonny Smith na Amadou Soukouna kuwafungia Tranmere.

Meneja Jurgen Klopp baada ya mechi alisema: "Makosa hutokea; Huwa siyapendi, na yeye pia hayapendi."

Mwezi Mei, Mjerumani huyo alifanya makosa mawili makubwa wakati wa fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ambapo walishindwa na Real Madrid.

"Kuwa na nguvu Karius, hili limewahi kutokea kwa wachezaji wazuri zaidi," ameandika Salah.

Karius alikuwa awali amejibu shutuma zilizoelekezwa kwake kupitia ujumbe kwenye mtandao wa Instagram.

"Kwa wale wanaofurahia kuwaona watu wengine wakishindwa au kuteseka, nawaonea huruma," aliandika.

"Kile kinachotokea katika maisha yenu kuwafanya kuwa na chuki na hasira kiasi hiki, naomba kipite na mambo mema yatendeke kwenu."

Meneja wa Liverpool Jurgen Klopp amemtetea Karius lakini akaonya kwamba kipa huyo ataendelea kukosolewa hadi pale atakapocheza vyema sana kwa mechi kadha.

Liverpool wameimarisha safu yao ya ulinda lango kwa kumnunua kipa wa Brazil, Alisson, kutoka klabu ya Roma ya Italia.

Comments

Popular Posts