Njia 13 za Kupata Usingizi Mzuri/Kulala Vizuri
Njia 13 za Kupata Usingizi Mzuri/Kulala Vizuri
Usingizi wa uhakika ni jambo jema sana kwa ajili ya afya ya mwili wako. Lakini kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, pamoja na kujengeka kwa jamii yenye mfumo wa maisha wenye shughuli nyingi, watu wengi hawapati usingizi mzuri.
Namkumbuka rafiki yangu mmoja alipata kazi nyingi sana kwenye mtandao. Hivyo ikamlazimu azifanye zote kwa muda mfupi bila kulala wala kula ipasavyo. Matokeo yake ameugua kwa miezi minne sasa na bado afya yake haijaimarika kama awali.
Hili linatupa umuhimu wa kuchunguza ni nini hasa manufaa ya kulala au usingizi mzuri?
- Huimarisha na kuboresha ukuaji wa mwili.
- Hujenga na kuimarisha kinga mwili.
- Hukuweka katika hali nzuri (mood).
- Hukuongezea kumbukumbu.
- Hurefusha maisha.
- Huboresha tendo la ndoa.
- Huondoa msongo wa mawazo.
1. Punguza mwanga wa rangi ya bluu jioni na usiku
Mwanga huu hupatikana hasa katika vifaa vya kielektroniki kama simu; kompyuta, televisheni n.k. Utafiti unaonyesha kuwa mwanga huu wa bluu hupunguza uzalishaji wa homoni ya “melatonin” ambayo ndiyo hutupa usingizi.Inashauriwa kuepuka kutumia mitandao ya kijaamii au kutazama vitu katika vifaa tajwa hapo juu usiku ili kuboresha usingizi wako.
2. Kaa kwenye mwanga wa kutosha mchana
Unapokaa kwenye mwanga wa kutosha mwili wako utaweza kutambua ni wakati upi umeamka na ni wakati gani wa kulala. Yaani mwili utatengeneza mazoea ya kubaini kuwa sasa ni usiku na ni wakati wa kulala kwani mchana kutwa hukuwa umelala.3. Epuka matumizi ya caffeine jioni au usiku
Sokoni leo vipo vinywaji kadha wa kadha vilivyotengenezwa au kuongezewa caffeine. Matumizi caffeine huamsha na kuchangamsha mwili wako na kuuweka katika hali ya kutojipumzisha.Hivyo matumizi ya caffeine jioni au usiku yatakupelekea kutopata usingizi mzuri. Vinywaji vyenye caffeine nyingi ni kama vile kahawa pamoja na baadhi ya soda Mf. Energy drink.
4. Punguza au acha kulala mchana
Mara ngingi unapolala mchana ni sawa na kusema umepunguza usingizi wa usiku. Kama siyo lazima kulala mara kwa mara mchana, basi ni vyema ukajitahidi kutolala ili kukupa usingizi wa uhakika na wa kutosha wakati wa usiku. Kumbuka, hakuna sababu ya kulala mchana wakati una usiku mzima wa kulala.5. Zingatia ratiba ya kulala na kuamka
Natumaini umewahi kulala zaidi ya muda uliozoea kuamka; na ulipoamka ulijihisi umechoka sana. Vivyo hivyo kwa siku uliyochelewa kulala pia. Hivyo basi, jitahidi kulala na kuamka kwa wakati unaofanana ili mwili wako uweze kufuata utaratibu ambao umeuzoea.Mwili unapobadilishiwa utaratibu wa kulala uliouzoea mara kwa mara ni dhahiri utakuonyesha matokeo hasi.
6. Usitumie kilevi/pombe
Kama nilivyoeleza katika hoja ya kwanza, “melatonin” ni homoni muhimu inayotuwezesha kulala. Utafiti uliofanyika umebaini kuwa uzalishaji wa homoni hii huathiriwa sana na matumizi ya pombe.Pombe ni kinywaji ambacho kimeonyesha kuwa na hasara nyingi katika mwili wa binadamu, hivyo ni vyema ukajitahidi kuepuka matumizi ya pombe.
Comments